Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae) - BONGO PUSH

Breaking

Opportunity First

Post Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 5 June 2019

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)


Katika mchakato wa kuomba ajira baada ya kuona tangazo la kazi, mambo matatu ni dhahiri. Mosi, huombi kazi hiyo wewe mwenyewe. Wapo watu wengi wanaoandika maombi na hivyo kuongeza ushindani wa nani atapata.

Pili, nyaraka unazotuma kwa mwajiri mtarajiwa ndizo zinazojenga utambulisho wako kabla wewe mwenyewe hujafahamika. Tatu, afisa mwajiri hatatumia muda mrefu kusoma maelezo yako. Katika hali ya kawaida, atatumia dakika moja kuamua ikiwa amevutiwa na maelezo yako ama la.

Kwa sababu hizo, maandalizi ya nyaraka utakazotumia kuomba kazi ni muhimu yafanyike kwa umakini ili kuongeza uwezekano wa kuitwa kwenye usaili.

Katika mfululizo wa makala hizi, tutajadili namna unavyoweza kuandaa nyaraka mbili kuu ambazo ni wasifu (maelezo) binafsi, pamoja na barua ya maombi ya kazi. Katika makala ya leo, tunaanza na wasifu binafsi. 

Wasifu binafsi ni maelezo yanayopambanua maarifa, ujuzi na uzoefu alionao mtafuta kazi kwa lengo la kumshawishi mwajiri kuwa anazo sifa na vigezo vya kuweza kufanya kazi iliyotangazwa.

Katika kuandika wasifu binafsi, mambo saba ni ya muhimu kuzingatia:


Taarifa za msingi za mtafuta kazi 


Weka taarifa zinazokutambulisha kama vile majina yako kamili, jinsia, hali ya ndoa, tarehe ya kuzaliwa, utaifa na njia muhimu za mawasiliano zinazoweza kutumiwa kukufikia. 

Mfano:
        Jina:
        Utaifa:
        Mahali pa kuzaliwa: 
        Tarehe ya kuzaliwa: 
        Hali ya Ndoa: 
        Anwani ya Posta: 
        Simu:
        Barua pepe: 

Hata hivyo, zipo taarifa nyinginezo zinazoweza kuwa muhimu lakini zisizo na ulazima wa kufahamika. Hizi ni kama kabila, dini, idadi ya watoto na mitazamo au ufuasi wa kisiasa.

Unaweza kuwa na aya moja yenye mhutasari wa wasifu wako, ukaeleza tunu zinazoongoza utendaji wako wa kazi. Aya hii inapoandaliwa vizuri hujenga taswira ya mtu anayejitambua.


Sifa za kitaaluma


Kuna namna nyingi za uandikaji wa sifa hizi, lakini kilicho muhimu ni kueleweka. Anza na ngazi ya juu zaidi ya kitaaluma uliyofikia na shuka mpaka ngazi ya chini. Onesha mwaka yalipofanyika mafunzo hayo, tunuku ya kitaaluma (mfano cheti, Stashahada, shahada) na chini yake taja taasisi iliyotoa tunuku hiyo na mahali ilipo (mfano shule, chuo na kadhalika).

Mfano;             
                          2011-2013: Shahada ya Sanaa katika Stadi za Mazingira
                                             Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi  

Kwa kawaida, sifa hizi huwa ni zile zinazohusiana na mafunzo ya ujuzi yatolewayo kwa ngazi ya chuo kukupa utaalam. Lakini waweza pia kutaja ngazi ya Cheti cha Juu cha Elimu ya Sekondari na Cheti cha Elimu ya Sekondari.


Uzoefu na historia ya kuajiriwa

Onesha ajira ulizowahi kuzifanya iwe kwa ajira rasmi au kwa kujitolea. Orodhesha uzoefu wako kwa mtiririko wa aina ya ajira kuanzia ya hivi karibuni zaidi au uliyonayo, taasisi husika pamoja na mwaka wa kuanza na kumaliza kazi hiyo.


Kumbuka kuwa mwajiri makini hutafuta kuona maneno muhimu kama "kuzalisha/kuongeza (ufanisi)", "kupunguza/kuondoa (changamoto)", "kubuni", "kuanzisha", "kusababisha", "kubadili", "kuchangia mabadiliko", "kuwezesha" na mengineyo.
Kwa mfano,
2013-2015: Mwandishi wa Habari za Mazingira, Mwananchi Communications Ltd
            Kwa kushirikiana na wenzangu, nilibuni utaratibu wa…ambao ulisaidia kuondoa changamoto ya…iliyokuwepo awali.

Usipoteze muda kueleza majukumu yako ya kila siku. Tafuta maeneo ambayo mchango wako ulionekana na yataje kwa kutumie vitenzi tulivyovitaja hapo juu. 

Ujuzi na weledi

Katika sehemu hii onesha aina ya ujuzi na weledi uliowahi kuupata kupitia warsha, semina na makongamano yalivyokusaidia kuongeza ujuzi mwepesi unaoweza kukusaidia "kuzalisha", "kukuza", "kubuni", "kuanzisha", "kusababisha", "kubadili", "kuchangia mabadiliko" na "kuwezesha". Onesha mahali, mwaka, shughuli husika na malengo yake kwa mtiririko wa kuanzia hivi karibuni mpaka yale ya zamani.


Machapisho na tafiti

Kama kazi unayoomba inahusiana na masuala ya taaluma na elimu (mfano ualimu, ukufunzi, utafiti, uhadhiri), onesha machapisho na tafiti ulizowahi kuzifanya na kuziandika. Hapa, utaonesha jina la chapisho husika, mchapishaji na mwaka lilipochapishwa. Lengo ni kuonyesha ushiriki wako katika kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili jamii, ikiwa ni pamoja na kuchangia kukuza maarifa yaliyopo.


Tuzo au heshima 

Mwajiri huvutiwa na mtu anayeweza kuonesha namna jitihada zake zilivyotambuliwa na wengine. Onesha namna bidii, na ari yako ya kazi ilivyowahi kutambuliwa katika ajira zilizopita. Si lazima iwe kazini tu, yaweza kuwa katika masomo, lakini ziwe tofauti na zile tunuku za kitaaluma moja kwa moja.

Maneno kama, "nilishinda", "nilituzwa" na "nilitambuliwa", kwa sababu ya shughuli, majukumu, jitihada zilizowahi kufanywa, yanakuongezea nafasi ya kukubalika.


Orodha ya wadhamini

Taja watu wanaoaminika wanaoweza kutoa ushuhuda wa uwezo na weledi wako. Orodhesha angalau watu watatu wenye nyadhifa zinazotambulika na wanaokufahamu vizuri iwe kwa sababu wamekufundisha au waliwahi kufanya kazi na wewe.

Ni vizuri kuwasiliana nao kabla ya kuwataja kwa kuwa wanaweza kuulizwa pasipo wewe kujua. Na wakati mwingine ni vyema kuwaomba kukuandikia barua ya utambulisho ukazitumia inapolazimika.


Zingatia
·         CV nzuri hubadilika kukidhi matakwa ya kazi inayoombwa.
·         Imeandikwa kwa ufupi na haizidi kurasa mbili
·         Ina taarifa nyingi muhimu lakini kwa maelezo yanayoonekana kirahisi
·         Imeandikwa kwa umakini na haina makosa ya kiuchapaji
·         Haina taarifa zilizotiwa chumvi au uongo
·         Haina picha ya mwombaji

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here